Ecclesiastes 2

Anasa Ni Ubatili

1 aNikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. 2 bNikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?” 3 cNikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu.

4 dNikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. 5Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. 6Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. 7Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike na watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ng’ombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. 8 eNikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia. 9 fNikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima.
10 Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani,
hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu.
Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote,
hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote.

11 Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo
mikono yangu ilikuwa imefanya
na yale niliyotaabika kukamilisha,
kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo;
hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.

Hekima Na Upumbavu Ni Ubatili


12 Kisha nikageuza mawazo yangu kufikiria hekima,
wazimu na upumbavu.
Ni nini zaidi mtu anayetawala baada ya mfalme
anachoweza kufanya ambacho hakijafanywa?

13 gNikaona kuwa hekima ni bora kuliko upumbavu,
kama vile nuru ilivyo bora kuliko giza.

14 hMtu mwenye hekima ana macho katika kichwa chake,
lakini mpumbavu anatembea gizani;
lakini nikaja kuona kwamba
wote wawili hatima yao inafanana.

15 iKisha nikafikiri moyoni mwangu, “Hatima ya mpumbavu itanipata mimi pia.
Nitafaidi nini basi kwa kuwa na hekima?”
Nikasema moyoni mwangu,
“Hili nalo ni ubatili.”

16 jKwa maana kwa mtu mwenye hekima,
kama ilivyo kwa mpumbavu,
hatakumbukwa kwa muda mrefu,
katika siku zijazo wote watasahaulika.
Kama vile ilivyo kwa mpumbavu,
mtu mwenye hekima pia lazima atakufa!

Kutaabika Ni Ubatili

17Kwa hiyo nikachukia maisha, kwa sababu kazi inayofanyika chini ya jua ilikuwa masikitiko kwangu. Yote hayo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. 18 kNikachukia kila kitu nilichokuwa nimetaabikia chini ya jua, kwa sababu ni lazima nimwachie yule ajaye baada yangu. 19Nani ajuaye kama atakuwa ni mtu mwenye hekima au mpumbavu? Lakini hata hivyo yeye ndiye atakayetawala kazi zote ambazo nimemiminia juhudi na ustadi chini ya jua. Hili nalo ni ubatili. 20Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi yangu yote niliyoifanya kwa taabu chini ya jua. 21Kwa kuwa mtu anaweza kufanya kazi yake kwa hekima, maarifa na ustadi, kisha analazimika kuacha vyote alivyo navyo kwa mtu mwingine ambaye hajavifanyia kazi. Hili nalo pia ni ubatili tena ni balaa kubwa. 22 lMtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua? 23 mSiku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili.

24 nHakuna kitu bora anachoweza kufanya mtu zaidi ya kula na kunywa na kuridhika katika kazi yake. Hili nalo pia, ninaona, latokana na mkono wa Mungu, 25kwa sababu pasipo yeye, ni nani awezaye kula na kufurahi? 26 oKwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
Copyright information for SwhKC